Luke 5:17-26

Yesu Amponya Mtu Mwenye Kupooza

(Mathayo 9:1-8; Marko 2:1-12)

17 aSiku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa. 18 bWakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya matofali, wakamteremsha yule mgonjwa kwa mkeka wake hadi katikati ya ule umati pale mbele ya Yesu.

20 cYesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”

21 dMafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

22Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 23Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 24 eLakini ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 25Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake, akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu. 26 fKila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”

Copyright information for SwhNEN